Maagizo ya daktari yasiyo ya kawaida |

Maagizo ya daktari yasiyo ya kawaida

Kutoka kwa Christian Science Sentinel Oktoba 4, 1900. Iliyoandikwa na Mhariri.


Katika toleo moja la juzi la Mlinzi, tulichapisha tena kutoka Midland tukio la binti mmoja aliyekwenda kwa daktari mmoja mwenye sifa mjini New York kupata ushauri wa matibabu. Baada ya kumpatia daktari orodha ya dalili za ugonjwa na kujibu maswali yake, aliambiwa anahitaji kusoma Bibilia yake zaidi. Wakati alipopinga, daktari alimwambia, kwa upole lakini kwa msimamo, aende nyumbani na kusoma Bibilia yake kwa lisaa limoja kwa kila siku kwa mwezi mmoja alafu aje kwake tena.

Alishangaa sana kwa ushauri huu ambao hakuutarajia kutoka kwa daktari wake, na mwishowe alihitimisha kwamba kwa sababu maagizo hayakuwa ya bei ghali angalao ajaribu. Mwisho wa mwezi alirudi kwa ofisi ya daktari na kutangaza ya kwamba alihisi kama mtu tofauti na hakuhitaji dawa ingine.

Alipoulizwa vile alijua yale matibabu ndio alihitaji, daktari alijibu ya kwamba angeacha kusoma Bibilia kila siku, angepoteza chanzo kikuu cha nguvu na ujuzi wake. Alisema ya kwamba hakuwai enda kufanya upasuaji au kushughulikia kisa cha kutatanisha bila kusoma Bibilia, alafu akaongezea: “ Kisa chako cha matibabu hakikudai madawa, lakini chanzo cha amani na nguvu nje ya akili yako, na nilikuonyesha mahali pa kuzipata bila kukosa. Nilikupatia maagizo yangu na nilijua itatibu.”

Alisema kulikuwa na visa nyingi katika kazi yake ambapo maagizo ile ingefanya maajabu, lakini ni wachache ambao walikuwa tayari kujaribu.

Maagizo kwa kweli hayakuwa ya kawaida kutoka kwa daktari, na lile ambalo linaweza kuwa kitu cha kushangaza ni kuwa ni maagizo ambayo daktari alikua ametoa kwa uhuru juu ya kisa chake. Kwa sababu alikuwa amesoma kutokana na uzoefu, alikuwa anajua anachokizungumzia.

Hata kama aliyepatiana maagizo alikuwa anategemea njia za maada na mbinu katika kazi yake, hata hivyo alihisi haja ya kutazamia chanzo cha juu zaidi kwa usaidizi. Hakuwa amefika mahali pa kuachana na mbinu za maada, lakini akatambua hii pekee haikutosha.

Ingawa inaweza kuonekana ya kwamba imani yake ilikuwa imegawanyika, bado angeishi kuendelea na kazi yake angefanya vile, bila shaka, angepunguza kutegemea mbinu za maada na kutegemea mbinu za kiroho pekee. Imani kama ile katika nguvu iliyo katika neno la Mungu haiwezi punguka lakini lazima iongezeke mpaka ionekane kuwa Mungu ni yote kwa yote.

Tukio laonyesha hamu kubwa ya wazo la kibinadamu kuinika juu ya vikwazo vyake na kupata msaada nje yake yenyewe. Njia na mbinu zake hushindwa wakati wa hitaji kubwa na inasikika kwa kina hitaji la kutazama zaidi ya njia na mbinu za kimwili kwa lile ambalo linaweza leta afya na furaha. Wanadamu wanawezaepushwa tajiriba nyingi zenye uchungu wakisoma mapema kugeuka kutoka duniani na kutazamia mbinguni.

Wanadamu hutambua kwa kiasi kidogo usaidizi ambao unapatikana kutokana na kusoma Bibilia kwa uaminifu. Tunaambiwa ya kwamba “ Maandiko yote yanapatianwa kwa himisho kutoka kwa Mungu.” Na kwamba “ watu wa Mungu waliokuwa watakatifu waliongea kama walivyoongozwa na Roho mtakatifu.” Kama haya ni kweli Bibilia iliandikwa kutoka kwa mtazamo wa juu zaidi kuliko vile dunia imefikia. Waandishi watakatifu walikuwa wamekaribia Ukweli wa Uwepo, ukweli wa uwepo wa milele, na vikwazo vya mawazo ya kibinadamu ilikuwa ilitoweka kwa kiwango.

Maneno ndio usemi wa mawazo, na kama msomi anafahamu mwandishi, anashiriki katika hali ya akili ya mwandishi. Bibilia ikisomwa kwa ufahamu, mawazo yanageuzwa kuwa ya kiroho na hii inaboresha hali ya mwanadamu kimaumbile na pia kitabia.

Dunia ya Kikristo imefunzwa, na imezoea kutazamia Bibilia kwa usaidizi wakati wa majaribu, lakini inashindwa kutambua ya kwamba ni usaidizi wakati wa magonjwa pia. Hii sio kwa sababu usaidizi haupo, lakini ni kwa sababu wanadamu hawatafuti wakitegemea kupata. Neno la Mungu haliongewi kwa upungufu kwa aliye mgonjwa kuliko kwa mwenye dhambi au Mkristo aliye na shida na huzuni. Inabaki kwa mwenye hitaji kutafuta kwa uaminifu na atapata.

Bibilia ni neno la Mungu kwa wana wake. Kwa sababu inakaa ngumu kutambua haya, ni vigumu kuamini kwa maneno yake, na kwa sababu hii ahadi zote haziwezi thibitishwa katika tajiriba ya kibinadamu. Lakini hii sio kwa kosa la Mungu, badala yake ni kosa la mwanadamu kuunyoosha mkono wake na kunyakua baraka ambazo ziko karibu naye. Kama wazo linageuka kuwa la kiroho, vikwazo vinavyowekwa na utafsiri wa kimwili wa neno la Mungu vinatolewa na baraka kuu za injili ya wokovu zinapatikana.

Mtunzi wa Zaburi aliimba: “ Mbariki Bwana, Nafsi yangu, na usisahau faida zake zote: ambaye husamehe dhambi zako zote: ambaye huponya magojwa yako yote.” Mnabii akasema “ Wamngojao Bwana watafanya upya nguvu zao; watapaa juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka; watatembea, na hawatazimia.” Tena, “ Mwangaza wako utang’aa kama asubuhi na afya yako kuchomoza kwa haraka.” Maandiko haya hayajapotoshwa wakati yanapotumiwa kwa uponyaji wa kimaumbile au wa kitabia, kwa sababu ni mapenzi ya Mungu ya kwamba mwanadamu awe mzima. Ikiwa mtu atafute na kutamani urejesho wa kitabia na wa kiroho kuliko uponyaji wa kimwili, bado hatakiwi kujipora mwenyewe kwa kupunguza nguvu za Mungu na utayari wa kutoa wema wote.

Anayeenda kwa Bibilia kama mtoto mdogo, akitamani kwa dhati kuelewa habari ya kimungu, atapata usaidizi. Hakuna jambo ambalo Mungu hawezi watendea wanae, na wale waaminifu, kusoma neno lake kwa waaminifu kunawezesha wanadamu kujifahamisha na Mungu na kuwa na amani.

Ugumu mkubwa umekuwa kwamba wakati wanadamu wanatambua lazima waamini ustawi wao wa kiroho katika utunzaji wa Mungu, wanaamini ufanisi wa mambo ya kimwili unategemea jitihada zao. Wanatakiwa kujua ya kwamba wao wenyewe hawawezi kufanya kitu na kwamba vitu vyote viko salama katika ”kiganja cha mkono wake.” Utafiti wa uaminifu wa Bibilia huvutia mtu na ukweli huu. Mungu yupo karibu na kuwa halisi zaidi kwa yule ambaye huasiliana naye zaidi na yu tayari kumuaminia mambo yote kwa utunzi wake.

Wanadamu hutambua kwa kiasi kidogo jinsi ilivyo ghala kubwa ya utajiri na hekima inayopatikana katika Bibilia. Nani anayethubutu kusema ya kwamba dunia haitakuwa bora, kwa kiasili na pia kitabia, kama maagizo haya yasiyo ya kawaida ya Daktari mwenye sifa wa New York yangetekelezwa kiulimwengu?

Wakati mtu anafungua Bibilia yake, na akumbuke ya kwamba “ Mungu hapendelei watu,” na kwamba habadilishwi, “ ni yule yule jana, leo na hata milele.” Alafu kama anasoma vile Mungu anajali wana wa Israeli, akikimu mahitaji yao yote, ya kimwili na pia ya kiroho; vile wema wake wa milele ulivyodhihirika nyakati za manabii; alafu kufikia siku za Yesu, tukikumbuka vile alivyowaponya wagonjwa na wenye dhambi na kutangaza ya kwamba “hakuja kuharibu lakini kutimiza ;” alafu tukikumbuka ya kwamba aliwatuma wanafunzi wake kwenye dunia yote kufanya kazi aliyofanya; tukikumbuka haya yote, tunauliza nani anayeweza kushindwa kuvutiwa na wazo lile, ya kwamba sisi wote ni wanae Mungu na habadiliki, kwa kweli lazima awe na uwezo na tayari kutubariki kama alivyofanya wale walioishi nyakati za Bibilia? Wakati wazo la kibinadamu linavutiwa kwa njia hii, nani anayeweza kuweka kikomo katika baraka ambazo zitatambulika na ambaye kwa mazoea anamgeukia Mungu?

Kama Wanasayansi ya Kikristo tunapenda Bibilia na kuthamini thamana yake kama haijawahi kuwa mbeleni, na mioyo yetu kujawa na shukrani kwa Mungu ya kwamba tuko na kitabu chetu cha kiada, “ Sayansi na Afya na ufunuo wa maandiko” iliyoandikwa na Mary Baker G. Eddy, kufafanua neno lake. Ni hazina kweli ambayo tuko nayo katika Bibilia na Sayansi na Afya, na rehema zake ni kuu kiasi kipi kwetu! Natusijiulize swali, tunathamini nafasi tukufu tumepatiwa kudhihirisha wema wa Mungu ambao unaongoza kwa toba? Je, tuko macho kwa ukweli ya kwamba tutawajibika kwa matumizi bora ya vipaji tulizopatiwa? Kama leo tunafurahia mwangaza mkuu kuliko jana, kazi kuu inatarajiwa kutoka kwetu na unyenyekevu zaidi wa akili ni muhimu kuitekeleza.